Makubaliano yenye utata ya kuwawezesha wanadiplomasia wa Ukraine kuingia nchini Afrika Kusini bila viza yamezua hasira katika ulimwengu wa kisiasa nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini Leon Schreiber, ambaye ni chama tofauti na rais, alitangaza mpango huo siku ya Jumapili, akiitaja Ukraine "mshirika wa thamani".
Lakini ofisi ya rais imemkosoa Schreiber kwa kutangaza makubaliano hayo bila idhini rasmi kutoka kwa Rais Cyril Ramaphosa.
Wakosoaji wanauchukulia mpango huo kama ukiukaji wa uhusiano wa muda mrefu wa Afrika Kusini na Urusi - ingawa nchi hiyo haijaegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine.
Chama cha African National Congress (ANC) kimetofautiana vikali na chama cha Democratic Alliance (DA), mshirika wake mkubwa wa muungano kuhusu uhusiano wa nchi hiyo na Urusi.
Chama cha ANC, ambacho kimetawala Afrika Kusini tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi miongo mitatu iliyopita, kilipoteza wingi wake katika uchaguzi mkuu wa Mei, na kulazimika kuingia makubaliano na vyama vingine vya kisiasa.
Waziri huyo wa mambo ya ndani wa nchi Leon ameweka wazi kuwaa ametia saini mkataba wa kihistoria unaowapa idhini kwa raia wa ukraine wenye hati za kusafiria za kidiplomasia kuingia afrika kusini bila visa.
Waziri alitetea uamuzi huo, akiangazia uungaji mkono wa Ukraine kwa Afrika Kusini wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Ofisi ya rais ilijibu na kusema kwamba tangazo la Waziri Schreiber lilikuwa la mapema kwani hakuwa na kibali kutoka kwa rais wa taifa hilo.
"Haijulikani ni jinsi gani waziri anaweza kutangaza saini ya makubaliano ya kimataifa bila idhini rasmi ya kufanya hivyo," msemaji wa Ramaphosa Vincent Magwenya alijibu kwenye mtandao wa X.
0 Comments