Chatanda awataka wanawake kuachana na mikopo Ujinga

 


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)Taifa,Mary Chatanda amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa ya mkopo usio na riba unaotolewa na Serikali ili  kuondokana na Mikopo ya Kausha damu, ujinga na mwendokasi inayo wanyanyasa na kuwadhalilisha Wanawake kutokana na utaratibu wa mikopo hiyo ikiwemo muda wa marejesho na kiwango cha Riba kuwa kikubwa hivyo badala ya kujikwamua kiuchumi inaongeza umasikini zaidi.

Chatanda amesema hayo jijini Dodoma leo wakati akizungumza na wafanyabiashara wanawake kabla ya kuzindua Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara Masoko yote Dodoma Jiji (UWAWAMA).

"Wanawake wenzangu,kama mnavyotambua Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imerejesha utoaji wa Mikopo ya Asilimia 10 kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kwa utaratibu ulioboreshwa Zaidi ikiwemo kutumia benki kwa Halmashauri 10 za majaribio ikiwemo za Dodoma.

"Hivyo natoa Rai kwa Wanawake wote wafanyabiashara kuchangamkia fursa hii kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo ya kuendeleza biashara zenu. Mikopo hii ni haki ya kila Mtanzania, sisi Wanawake tumepata bahati hii kubwa ya kupewa kipaumbele,"amesisitiza Chatanda. 

Aidha amewapongeza wanawake hao kwa uamuzi waliyoufanya wa kuanzisha umoja wa Wanawake Wafanyabiashara Masoko yote Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kusajili rasmi,ambapo amesema Umoja huo utaendelea kuimarisha ushirikiano wa Wafanyabishara Wanawake. 

"Kwa kasi hiyo natumai Dodoma Jiji mtakuwa wa Mfano kwa kuchangamkia fursa za mikopo ya Halmashauri. Nyinyi Wanawake wa Dodoma mkifanya vizuri hata Mikoa mingine watajifunza kutoka kwenu,"amesema Chatanda.

Vilevile ametumia fursa ya mkutano huo kuziomba Halmashauri kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanawapatia Mafunzo ya elimu ya Ujasiriliamali kwa vikundi vyote vinavyoomba mikopo kabla ya mikopo kutolewa ili pesa zinazopatikana ikatumike kwa iliyokusudiwa na kuwasihi kutoa kipaumbele kwa vikundi vyenye sifa na watakaoonyesha nia thabiti katika kujijenga kiuchumi.

"Natoa wito kwa Viongozi wanawake kuhamasisha walengwa wa mikopo hii wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali yao,lakini pia nitoe rai kwa Halmashauri zote zihakikishe mikopo hii inawafikia walengwa bila ubaguzi au upendeleo wa aina yeyote.

"UWT inaishauri Serikali kutoivumilia Halmashauri yoyote nchini ambayo haitatekeleza kwa uadilifu zoezi hili la utoaji Mikopo ya asilimia kumi.

Sambamba na hayo Chatanda amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),Mohamed Mchengerwa,Wizara ambayo inasimamaia Uchaguzi wa serikali za mitaa inaonesha wanawake walioandikishwa ni asilimia 51.29 na asilimia 48.71 ni wanaume.

Hivyo, kutokana na idadi hiyo kubwa ya wanawake waliojitokeza,Chatanda aliwapongeza nakuwaomba wanawake na wananchi wote baada ya michakato ya uchaguzi inayoendelea,kwenda kushiriki kupiga kura siku ya tarehe 27/11/2024.

Ambapo amesema uchaguzi huo ni muhimu kwa kila mwananchi kushiriki kuchagua viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwani ndio viongozi wa kwanza pindi inapohitajika huduma ya Serikali, hivyo viongozi watakaochaguliwa tarehe 27/11/2024 ndio watakaoonesha sura ya Serikali, na hata maendeleo yanayoonekana ngazi ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji, ni kazi nzuri inayofanywa na viongozi hao.

Mwandishi.  Zena Mohamed, Dodoma

Post a Comment

0 Comments