DKT. BITEKO AIPONGEZA DODOMA JIJI KUVUKA LENGO UANDIKISHAJI WAPIGA KURA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuandikisha idadi kubwa ya wananchi katika daftari la wapiga kura ikiwa ni maandalizi ya Uchanguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024. 

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo Novemba 10, 2024 wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi wa Jimbo la Dodoma Mjini uliyolenga kutoa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa Mwaka 2020 hadi 2024.

“Kipekee kabisa niwapongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufanya vizuri zaidi kuliko Halmashauri yoyote nchini kwa uandikishaji uliovuka lengo mpaka kufikia asilimia 128 ya lengo la uandikishaji. Hii ni kuthibitisha kwamba Mkoa wa Dodoma mmejipanga vizuri sana kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao,” amesema Dkt. Biteko.

Pia, Dkt. Biteko ametoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo imeleta manufaa makubwa katika ustawi wa jiji la Dodoma.

“Ninampongeza sana Mbunge wenu Mhe. Anthony Peter Mavunde kwa tukio la leo la uwasilishaji wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024 pamoja na kukabidhi vitendea kazi kwa viongozi kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nimefurahishwa kwa namna ambavyo zimefanyika kazi kubwa za kugusa maisha ya watu na hasa watu wenye kipato cha chini na kuwa karibu na wananchi,” amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza “Nataka niwaambie watu wa Dodoma Mhe. Mavunde ana sifa nyingi nataka nitaje chache, Mbunge wenu anajua ubunge alionao si wake ni wa CCM na wanachama wake hivyo wakati wote amekuwa mtu anayeshughulika na shida za watu, mtu anayefanya kazi na anastahili kuambiwa akiwa hai yeye anafanana na watu walipewa talanta na yeye anafanana na aliyepewa talanta tano,”
Pia, Mhe. Mavunde amesema kuwa Jimbo lake lilikuwa na changamoto kubwa ya ardhi lakini kupitia kliniki za ardhi zilizofanyika zimesaidia kutatua changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainab Katimba amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa katika Jimbo la Dodoma Mjini hususan katika miundombinu ya barabara.

“Katika miundombinu ya barabara mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka minne tumeona ongezeko la bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 5.3 hadi 42.6 kwa mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu, hii ni dhamira ya dhati ya Rais kuona Dodoma inapata miradi ya kimakakati,” amesema Mhe. Katimba.

Amebainisha “ Sasa TARURA inaweza kuhudumia mtandao wa barabara za lami kutoka urefu wa km 154 hadi  km 249 na barabara za changarawe kutoka km 196.4 hadi km 368.2 hapa Dodoma Mjini, imejenga  makaravati 9 pamoja na kupamba jiji hili kwa taa za barabarani 243.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini, Charles Mamba amesema kuwa mkutano huo ndio ulimpendekeza Mhe. Anthony Mavunde kufanya kazi za kibunge na kupitia mkutano huo pia ataeleza yale ambayo ametekeleza katika Jimbo hilo.

Ameongeza kuwa Dodoma Mjini wako tayari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wamedhamiria kushinda nafasi za uenyekiti kwa asilimia 100.

Awali, Dkt. Biteko amekabidhi  baiskeli 223 kwa makatibu wa matawi wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na spika 45 kwa makatibu kata wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Dodoma Mjini ikiwa ni jitihada za Mbunge wa Jimbo hilo kusaidia viongozi hao kuwafikia wananchi kwa urahisi pamoja na kuwezesha ufanyikaji wa mikutano ya hadhara kwa wananchi.

Na mwandishi wetu 
Mhariri : Abel  Mahenge

Post a Comment

0 Comments