Hali bado tete Msumbiji.

 

Polisi nchini Msumbiji wakisaidiwa na wanajeshi walitumia mbwa na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji kwenye mji mkuu, Maputo, jana Alhamisi walioingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi yanayozozaniwa.

Taifa hilo la kusini mwa Afrika limeingia kwenye machafuko tangu kutangazwa kwa  matokeo ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9 yaliyompa ushindi wa asilimia 71 mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo.

Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, amedai matokeo ya uchaguzi wa rais yalikuwa ya udanganyifu na kwamba yeye ndiye mshindi, aliitisha maandamano hapo jana akisema ni muhimu kwa mustakabali wa taifa hilo.

Maelfu ya wafuasi wake waliingia mitaani kupinga matokeo hayo baadhi wakirusha mawe na kuweka vizuizi njiani kwa kuchoma matairi na mapipa ya taka. Maduka, mabenki, shule na vyuo vikuu vilifungwa mjini Maputo.


Waandamanaji ndani ya mji mkuu wa Maputo wakichoma tairi nakuweka vizuizi njiani kuonyesha kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi.

Polisi waliojihami kwa silaha na magari ya kivita waliwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu na baada ya saa kadhaa hali ya utulivu ilirejea.

Makundi ya kutetea haki yanasema takriban watu 18 wameuwawa katika operesheni hizo za polisi katika maandamano yanayopinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 9 ambao umeongeza utawala wa chama cha Frelimo kwa miongo mitano.

Vyama vya upinzani, makundi ya jamii na waangalizi wa kimataifa wamesema uchaguzi haukuwa haki na matokeo yalichujwa.

Afrika Kusini imefunga mpaka wake mkubwa siku aya Alhamis kwa sababu za kiusalama, na kuwashauri raia wake kutofanya safari zote zisizokuwa na umuhimu kwenda Msumbiji.

Kampuni ya usafirishaji ya Afrika Kusini siku ya Alhamis imesimamisha shughuli za bandari nchini humo.

Baraza la Katiba wiki hii limeiamrisha tume ya uchaguzi kutoa maelezo kwa nini kumekuwa hakuna uwiano wa idadi za kura zilizohesabiwa katika uchaguzi, kulingana na barua iliyoonekana kwa shirika la habari la Reuters.

Mwandishi:Eunice Jacob.

Muhariri:Ramadhani Zaidy.

Post a Comment

0 Comments