Waziri Mkuu wa Lebanon ameituhumu Israel kwa kuukataa mpango wa kusitishwa mapigano kati yake na Hezbollah. Hii ni baada ya jeshi la Israel kuilipua ngome ya Hezbollah kusini mwa Beirut kwa mara ya kwanza wiki hii.
Waziri Mkuu Najib Mikati amelaani kile alichokiita "utanuzi" wa mashambulizi ya Israel, akisema yanaashiria kukataa kwake kushiriki katika mazungumzo ya kuweka chini silaha.
DW imeripoti kuwa karibu mashambulizi 10 ya anga yalivipiga vitongoji vya kusini kabla ya alfajiri Novemba 1 baada ya Israel kutoa maagizo ya kuwataka wakaazi wahame.
Mashambulizi hayo yamejiri siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukutana na maafisa wa Marekani kujadili uwezakano wa makubaliano ya kumaliza vita nchini Lebanon, kabla ya uchaguzi wa rais nchini Marekani Jumanne ijayo.
Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya Israel katikati mwa Gaza yamepanda hadi watu 25, wakiwemo watoto watano, huku watu 13 wameuawa leo katika mashambulizi ya anga nchini Lebanon, Watu 16 walikuwa wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi mawili jana Alhamisi katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati ya Ukanda wa Gaza.
Mhariri; Sharifat Shinji
0 Comments