Jamii imetahadharishwa kuepuka ulaji usiozingatia makundi sita ya chakula kwani unasababisha Ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) ambayo yanaongezeka katika jamii kwa kasi.
Akizungumza na
Buha News, Mratibu wa elimu ya afya kwa Umma Halmashauri ya mji Kasulu, Mkoani
Kigoma Mwita Range, amesema kwasasa magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) yamekuwa
yanaongezeka kwa kasi katika vituo mbalimbali vya afya ikiwa ni Matokeo ya Mtindo
wa maisha wa jamii.
“Hivi Karibuni Katika vituo vyetu vya afya kumekuwa na ongezeko la wateja wanaofika wakisumbuliwa na maradhi haya, yasiyo ya kuambukiza na kwa bahati mbaya magonjwa haya hayana matibabu ya moja kwa moja, kwahiyo Kitu kikubwa cha kuzingatia ni kuepuka visababishi vyake kwa kula mlo wenye Wanga ,protin,mbogamboga,Matunda na mafuta na sukari kwa kiwango kidogo” amesema Mratibu wa elimu ya afya kwa Umma Mwita Range.
Mratibu huyo wa elimu ya afya kwa umma, amesema mlo usiozingatia makundi sita ya chakula na kutokufanya mazoezi ni chanzo kikubwa cha ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) ikiwemo Kisukari,Kansa na magonjwa moyo.
“Watu wengi kwasasa wanatumia zaidi vyakula vya viwanndani au vyakula vilivyopitia mchakato mrefu ambavyo vikiliwa kwa wingi zaidi ya vyakula vya asili vinasababisha Magonjwa yasiyo ambukiza, pia watu wanatumia zaidi vyombo vya usafiri na hawafanyi mazoezi hii ni hatari” ameongeza Mratibu wa elimu ya afya kwa Umma Range
Bw.Range amesema mtu akishindwa kabisa angalau ale
makundi manne ya siku,alafu makundi mengine anaweza kuyatumia siku inayofuata, Pia ameshauri wananchi kuzingatia matumizi ya chumvi yenye madini
chuma na kuwa na tabia ya kupima afya angalau mara moja kwa
mwaka.
“Magonjwa yasiyoambukiza hayana dalili za
haraka,yanaweza kutambulika hata baada
ya miaka 5 hivyo nishauri watu kuhakikisha wanapima afya zao angalau mara moja
kwa mwaka”
Hata hivyo baadhi wa wananchi waliohojiwa na Buha News mjini Kasulu ambao hawakupenda kutaja majina yao,
walikiri kusikia na kuona wagonjwa wenye Kisukari na moyo japo hawakufahamu juu
ya chanzo cha magonjwa hayo.
"Mimi binafsi sijui kama yanauhusiano wa chakula na
wala sijui chanzo chake ila nimeona wagonjwa wa Kisukari,ugonjwa wa moyo
nasikia unasababisha na msongo wa mawazo” alisema moja ya wananchi hao.
Januari 10 mwaka huu Waziri wa Afya kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui wakati wa Uzinduzi wa Utafiti wa Kitaifa wa Viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza (STEPS SURVEY 2023) uliofanyika kwenye ukumbi wa Tawimu Jijini Dodoma alisema
Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) yanachangia takribani asilimia
33 ya vifo vyote nchini huku kwa takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) kwa
mwaka 2020 zinaonesha kuwa magonjwa hayo yalichangia zaidi ya vifo milioni 41
sawa na asilimia 71 ya vifo vyote Duniani ukilinganisha na vifo milioni 57 kwa
mwaka 2016 duniani.
Mhe. Mazrui alisema takwimu zinaonesha kuwa magonjwa
hayo yameongezeka mara 5 hadi 9 zaidi kati ya miaka ya 80 ambapo asilimia 1 tu
ya watanzania walikuwa na tatizo la kisukari na asilimia 5 walikuwa na tatizo
la shinikizo la juu la damu wakati kwa sasa tatizo la kisukari limefikia
asilimia 9 na tatizo la shinikizo la juu la damu limeongezeka na kufikia
asilimia 25.
Mwandishi; Harieth Dominick
Mhariri; Ramadhani Zaidy
0 Comments