Mfumo wa elimu nchini wakosolewa

 


MBUNGE wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha, amekosoa mfumo wa elimu kuwa ni tatizo kutokana na masomo kufundishwa "kijumla jumla" na kutokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kupunguza umaskini.

Akichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26, amesema njia mwafaka ya kuongeza tija katika uzalishaji iwe katika sekta ya kilimo au viwanda ni kuwekeza kwenye elimu bora inayosisitiza ufundi na ugunduzi.

“Tatizo letu ni nini, tunafundisha masomo ya jumla jumla ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja katika kupunguza umaskini, nilitarajia tungefundisha usimamizi wa mipango, usimamizi wa maendeleo, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa viwanda na usimamizi wa sekta ya afya na ndiyo ambayo yanahusiana na kupunguza umasikini.”

Vile vile, amesema alitarajia wafundishwe masomo ya ukalimani, ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni ili watafsirie wataalamu nchi za ughaibuni na kwa upande wa teknolojia alitarajia wafundishwe vijana masuala ya sayansi ya data na akili bandia.

Amesema Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kina shule nzima ya teknolojia ya habari na wakati huo huo Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari inajenga chuo cha umahiri cha teknolojia na Tehama na kudai kuwa ni matumizi mabaya ya fedha.

Naye Mbunge wa Mahonda (CCM), Abdullah Ali Mwinyi, alisema elimu ya chuo kikuu haina umuhimu mkubwa kwenye ajira na kampuni zote kubwa kwa kuwa wanaangalia suala la ujuzi.

Mwandishi : Abel  Mahenge 

Mhariri :Eunice Jacobo 

Post a Comment

0 Comments