Wananchi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa kusikiliza sera ili kujua nia za wagombea na vyama vyao na kisha wachagua viongozi makini na wenye ya maendeleo badala ya kuchagua viongozi kwa urafiki au kushawishiwa kwa rushwa.
Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Kigoma Mhe. Zaituni Buyogela wakati wa kampeni katika Kijiji wa Mvinza na Kagerankanda katika Hakmashauri ya wilaya ya Kasulu.
Mhe. Buyogela amesema Tanzania bado ni nchi inayoendelea hivyo inahitaji kuwa na viongozi makini katika kila eneo, hivyo ni wajibu wa wananchi kuhakikisha wanasikiliza sera makini kutoka kwa wagombea na si sera za uchochezi.
Amesema Kata ya Kagerankanda ni miongoni mwa maeneo ambayo wanawake wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi katika nafasi zote na ni kawaida kwa CCM kuwapa nafasi wanawake huku akisisitiza waaminiwe na wapewe nafasi kwani wanaweza.
“Kata ya Kagerankanda ina jumla ya wananwake nane waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hili si la ajabu katika chama cha mapinduzi (CCM) hivyo ninawaomba wananchi wa Kagerankanda na maeneo mengine nchini kuwaamini na kuwapa nafasi wagombea wote wa chama cha mapinduzi” amesema Mhe. Buyogela.
Ameongeza kuwa kata ya Kagerankanda ni kata yenye miradi mingi ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji ambao umegarimu zaidi ya shilingi Bilioni moja, ujenzi wa Shule na sasa mchakato wa ujenzi wa zahanati umekamilika na wakati wowote ujenzi unaanza.
Ametaja sababu ya kata hiyo kuwa na maendeleo hayo nimkutokana na kuwa na viongozi makini ambao wameaminiwa na wananchi pamoja na serikali kuu kuwatumikia wananchi ndio maana miradi kama hiyo inajengwa.
Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Kigoma Mhe. Zaituni Buyogela akisalimiana na wananchi wakati wa kampeni.Aidha amesisitiza wananchi kujitokeza siku ya uchaguzi kwa wingi ili kuwapigia kura viongozi walionadi sera za Upendo, Mshikamano bila ya kuacha maendeleo ya wananchi huku akisisitiza amani na utulivu.
Uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika jumatano Novemba 27 mwaka huu na nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Kijiji, Mtaa, Kitongoji na wajumbe wa serikali katika ngazi hizo.
Mwandishi: Mussa Mkilanya
Mhariri: Prosper Kwigize
0 Comments