Msemaji wa Simba SC Ahmed Ally leo ameungana na Wanasimba wengine Karume kuchangia damu kwa watu wenye uhitaji.
Zoezi hilo la uchangiaji damu ni sehemu ya hamasa kuelekea katika michuano ya kombe la shirikisho barani Africa ambapo Simba watarusha karata yao ya kwanza uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam dhidi ya Bravos ya nchini Angola.
“Tarehe 27 tuna jambo kubwa kwenye Uwanja wa Mkapa. Tunahitaji kuanza vizuri hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ushindi wa Simba unakutegemea wewe Mwanasimba, tambua ya kwamba tiketi utakayonunua ni silaha muhimu ya kuisaidia Simba siku hiyo.”
Ahmed Ally amesema kuwa siku ya kucheza itaangukia tarehe ya uchaguzi wa serikali za Mitaa na kuwahasa mashabuki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura kutimiza haki zao kikatiba.
“Tunatambua siku hiyo ni siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ukishamaliza kupiga kura yako elekea Uwanja wa Mkapa. Asibaki Mwanasimba siku hiyo, tambua kwamba ushindi wa Simba unapatikana kwa ushirikiano wa nguvu wa kila Mwanasimba.”
Amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuwapa hamasa wachezaji wao ilikupata matokeo rafiki yenye kuwapa matumaini ya kutimiza malengo Yao ya msimu wa 2024/2025 kimataifa ya kufika fainali ya michuano hiyo ya kombe la shirikisho Afrika.
“Tumejiandaa siku hiyo kila Mwanasimba atakayekuja uwanjani aondoke na furaha. Tumedhamiria msimu huu kila anayekuja lazima tumfunge. Kwahiyo ndugu zangu Wanasimba jukumu letu la msingi ni kwenda uwanjani na ukienda uwanjani usitulie, unafanya balaa unaloweza.”
Simba SC wanahitaji kuvunja mwiko wakuishia hatua za robo fainali katika michuano ya kimataifa wapo kundi A na timu za Bravos do Maquis, CS Sfaxien, Constantine wataanza michuano hiyo Jumatono Nov 27 mwaka huu.
Mwandishi:Eunice Jacob
Mhariri: Abel Mahenge
0 Comments