MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, ameingilia kati malalamiko ya vyama vya upinzani kudai wagombea wao wameenguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupuuza kasoro ndogo ndogo zilizofanywa na wagombea wa vyama vya siasa wakati wa kujaza fomu kwa ajili ya uchaguzi huo unaohusu serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwapo wa wagombea wengi wa vyama vya siasa kuenguliwa kutokana na makosa madogo waliyoyafanya wakati wa kujaza fomu.
"Nilikuwa na kikao na Mwenyekiti wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameiagiza TAMISEMI kuyapuuza makosa madogo madogo yaliyojitokeza wakati wa kujaza fomu.
CCM inaamini katika demokrasia, hivyo ni wakati wa kuwapa nafasi wale waliokosea kujaza fomu kwa makosa madogo madogo," alisema.
Dk. Nchimbi amesema kuna makosa makubwa ambayo hayakwepeki ambayo TAMISEMI inapaswa kuzingatia sheria, akitolea mfano mgombea kujaza fomu au kushiriki katika kundi la jinsia nyingine.
Amesema lengo la Dk. Samia ni watu wapate nafasi zaidi ya kujifunza kwamba demokrasia ya nchi bado changa pamoja na kila Mtanzania (mgombea) apate nafasi ya kulitumikia taifa.
Nchimbi alisema idadi ya mitaa nchini ni 4,265 lakini wapinzani wamesimamisha wagombea 3,256 na CCM wagombea 1,009.
Aidha nchimbi Amesema idadi ya vijiji nchini ni 12,274 vyama vya upinzani vimesimamisha wagombea 5,889, vitongoji ni 63,863 vyama vya upinzani vimesimamisha wagombea 20,000 na CCM wagombea 42,000.
Mwamdishi: Abel Mahenge
mhariri : Eunice Jacobo
0 Comments