Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola amekubali kuongeza mkataba wa mwaka mmoja katika klabu ya Manchester City.
Ingawa City wamekataa kuzungumzia habari hiyo iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la The Athletic, vyanzo vingi vimethibitisha kuwa Guardiola amechagua kusaini mkataba mpya, utakao mfanya kuwepo katika klabu hiyo kwa miaka 10.
Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 53 alijiunga na City mwaka 2016 na ameshinda mataji 18 hadi sasa, yakiwemo mataji sita ya Ligi Kuu ya England.
Mkataba wake ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Wakati akiwa Manchester City, Guardiola ameisaidia timu hiyo kuwa timu ya pili ya wanaume ya Uingereza kushinda makombe matatu katika msimu mmoja, ligi kuu ya England, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia City imekuwa timu ya kwanza ya wanaume kushinda mataji manne mfululizo ya ligi kuu ya England na kufikia pointi 100 za ligi hiyo katika msimu mmoja.
City wanashika nafasi ya pili kwenye Ligi ya England msimu huu, pointi tano nyuma ya vinara Liverpool, baada ya City kupoteza michezo minne mfululizo.
Mhariri:Eunice Jacob.
0 Comments