Siku ya UKIMWI Dunia Kitaifa kufanyika Mkoani Ruvuma

 



Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo huadimishwa Desemba Mosi  kila mwaka na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa mwaka huu 2024 yanatarajiwa kufanyika kitaifa katika viwanja vya Majimaji mkoani  Ruvuma kuanzia tarehe 24 Novemba hadi 1 Desemba, 2024.

 Hayo yamesemwa  Novemba 14, 2024 Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga katika mkutano wake na Waandishi wa Habari kuekea maandalizi  ya siku ya UKIMWI Duniani Kitaifa. 

 Mhe. Nderiananga amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki kwenye ajenda ya udhibiti UKIMWI ambayo ni ajenda ya kidunia, kutathmini muelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI nchini na kutafakari changamoto mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya udhibiti wa Virusi vya UKIMWI(VVU).

 "Timu yetu kupitia TACAIDS tumeendelea kuwasiliana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma, hivyo nitoe wito kwa Watanzania wote na wana Ruvuma kuhakikisha tunashiriki vizuri pia niwahimize wadau wote chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea  na maandalizi ya maadhimisho hayo," amesema Mhe. Nderiananga.


Waandishi wa Habari kutoka vyombo vya Habari mbalimbli wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga katika mkutano wake.

 Pia Mhe. Nderiananga amesema kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI mikoa yote nchini imeelekezwa kuandaa na kuadhimisha siku ya UKIMIWI Duniani ifikapo  Desemba 1, 2024 katika mikoa yao nchi nzima.

"Nichukue fursa kuendelea kuwahimiza wakuu wa mikoa yote kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mikoa yao kusimamia utekelezaji wa shughuli hii na kuhamasisha wananchi katika ngazi zote kwa pamoja tushirikiane kuadhimisha siku hii," amesema Mhe. Nderiananga.

Aidha mh nderiananga amesema serikali imefanya jitihada kubwa za kupunguza maambukizi mapya ya VVU kutoka watu 72,000 mwaka 2016/2017 hadi kufikia watu 60,000 mwaka 2022/23 na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa asilimia 67 kutoka 2010.

 

Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Kaimu Mkuu wa Program Dkt. Riziki Kisonga amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wadau imejipanga kutoa huduma mbalimbali katika maadhimisho hayo kuanzia Tarehe 24 Novemba mpaka siku ya kilele tarehe 1 Desemba, 2024.

"Huduma ambazo tutazitoa zinahusisha huduma za elimu juu ya Virusi vya UKIMIWI (VVU) na matumizi sahihi ya dawa na kingatiba kwa makundi maalum bila kusahau watoto waliopo katika mazingira hatarishi ya kupata UKIMWI, upimaji wa VVU na magonjwa muambata ikiwemo magonjwa ya ngono na homa ya ini," amesema Dkt. Kisonga.

 Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kwa mwaka 2024  ni  'Chagua njia sahihi tokomeza UKIMWI'.

Mhariri: Harieth Dominick

Post a Comment

0 Comments