Simba yakwea kileleni Ligi Kuu na rekodi kibao


WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imesimama kupisha michezo ya timu za taifa huku timu ya simba  ikiongoza kwenye msimamo kwa kuwa na pointi 25, Simba ina rekodi nyingine nyingi za kuvutia mpaka sasa.

Kwa mujibu wa dawati letu la takwimu, Simba imefunga mabao 21 na kuwa timu pekee iliyopachika mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa.

Simba pia ina rekodi ya kukusanya pointi nyingi ikiwa nyumbani kuliko timu nyingine yoyote ambapo kati ya pointi 25 ilizonazo, 13 imezipata ikicheza michezo ya nyumbani.

Timu hiyo imecheza mechi sita ikiwa nyumbani na kufanikiwa kushinda mechi nne, imetoka sare na kupoteza mchezo mmoja.

Simba ilianza Ligi kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, ikapata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Fountain Gate, ikazifunga Namungo FC mabao 3-0, KMC mabao 4-0, huku ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union na kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Takwimu zinaonyesha imefunga mabao mengi kuliko timu yoyote ikicheza nyumbani, ikiwa imepachika mabao 16.

Timu hiyo imecheza mechi nne tu ugenini ambapo imeshinda zote na kukusanya pointi 12.

Michezo minne ambayo imecheza ikiwa ugenini ni dhidi ya Azam FC ikishinda mabao 2-0, ikazifunga Dodoma Jiji bao 1-0, Mashujaa FC 1-0 na Prisons 1-0.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, alisema mpaka wanakwenda mapumziko ameridhishwa kwa kiwango cha wachezaji wake, lakini akisisitiza kuwa bado hakijafika sehemu ambayo anataka.

"Nadhani hapa iko kwenye asilimia 55 tu, kuna kitu ambacho nakihitaji sijakiona. Kuna vitu vingine tumefanya vizuri, ikiwemo baadhi ya wachezaji kuanza kujiamini, timu imeanza kuwa na muunganiko mzuri, wameanza kuelewana, mmoja akiwa na mpira wanajua mwenzake anaweza kuwa wapi, mikimbio yake ni ipi, anakwenda kasi au taratibu, hili tumeshafanikiwa, nilikuwa pia nataka wachezaji wanaobaki benchi nao wawe msaada kwenye timu, nimeanza kuona, lakini kiufundi kuna vitu havijakaa sawa, ikiwemo kasi kwa dakika zote 90, kikikaa mabadiliko yataonekana." alisema Fadlu raia wa Afrika Kusini.

Kikosi cha Simba kwa sasa kimerejea mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquis unaitarajiwa kuchezwa Novemba 27, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Mwandishi: Abel Mahenge 

Mhariri : Ellukagha  kyusa 

Post a Comment

0 Comments