Ukikatwa CCM, kaa kimya


 KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuwa na subira.

Amesema watakaokatwa licha ya kushinda kura za maoni, wasiseme neno, badala yake wawe na uvumilivu kwa kuwa muda wao utafika, huku akiwatakia heri waliohamia vyama vingine, akidai kuwa ni suala la muda tu.

Mwenezi huyo pia amesema uchaguzi wa awamu hii hauna kupita bila kupingwa, hivyo wagombea na wanachama wa chama hicho wasibweteke, akisisitiza wako imara na hawatalala.

Makalla ameyasema hayo  mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa chama wilayani Kinondoni, akisisitiza watahakikisha hata pale watakapokuwa peke yao, watafanya kampeni na kuhakikisha wagombea wao wanapata kura za "ndio".

"Niwaombe tuendelee kufuatilia viongozi wetu wa matawi, kata, wilaya na mkoa, michakato inayoendelea sasa ya kupeleka wagombea katika maeneo hayo, itakapofika Novemba 21, mwaka huu tuanze kampeni za kistaarabu za kunadi mafanikio tuliyonayo na utekelezaji ilani ya uchaguzi. Kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ni mtaji tosha wa kuipa CCM ushindi," alisema Makalla.

Ameongeza kuwa wamefanya hamasa kubwa ya uandikishaji iliyofanikisha zaidi ya watu milioni tatu kuandikishwa ndani ya mkoa wa Dar es Salaam pekee, akieleza kuwa hamasa hiyo itakayotumika kufanya kampeni muda utakapofika, ifanywe kuwasisitiza wananchi kutoishia kwenye kijiandikisha badala yake wajitokeze pia kupiga kura.

Makalla ameeleza kuwa chama hicho kinaamini kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu, hivyo wamejiwekea utaratimu maalumu ambao ulifanikisha kupata zaidi ya viongozi 500 watakaogombea katika maeneo mbalimbali kote nchini, akiwasisitiza kuonesha taswira nzuri kwa kuwa wameaminiwa.

Amewapongeza baadhi ya wagombea ambao majina yao yalikatwa na wanaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za chama hicho, akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuna kipindi aligombea na kushinda kwa kishindo lakini jina lake halikurudi.

Mwandishi : Abel  Mahenge. 

Mhariri : Ellukagha Kyusa.

Post a Comment

0 Comments