Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland imeandaa Mkutano wa Kikanda kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unaohusu masuala ya Matumizi Bora ya Nishati.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mkutano huo wa kikanda kwa Waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.Mhandisi Luoga amesema kuwa, mkutano huo utakaofanyika tarehe 4-5 Desemba 2024, jijini Arusha unatokana na programu ya pamoja ya Serikali ya Tanzania, UNDP, EU na Ubalozi wa Ireland inayohusika na Matumizi Bora ya Nishati iliyoanza kutekelezwa mwaka 2022.
Amesema katika Mkutano huo, ujulikanao kama Regional Energy Efficiency Conference (REEC) ambao mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko unahusisha wadau wa nishati takriban 400 wa ngazi mbalimbali ikiwemo Mawaziri, wataalam na sekta binafsi, utajumuisha kubadilishana uzoefu na uelewa katika masuala ya nishati, fursa zilizopo na uwekezaji.
Akizungumzia pogramu ya Matumizi Bora ya Nishati, Mhandisi Luoga amesema ina umuhimu mkubwa nchini kwani inahusisha matumizi ya umeme kwa ufanisi na kwa ubora, inalenga kupunguza upotevu wa umeme, kupunguza gharama za umeme na kulinda mazingira.
Kuhusu utekelezaji na faida za programu hiyo, Mhandisi Luoga amesema Tanzania tayari imeshaandaa mkakati wa matumizi bora ya nishati wa miaka 10 (2024-2034), kumekuwa na ufadhili wa wanafunzi wa kike katika masuala ya nishati, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeshaanza kuandaa viwango vya matumizi bora ya nishati kwenye vifaa mbalimbali kama majokofu, pia kuna vijana takriban 152 wamepata ufadhili kutokana na ubunifu katika matumizi bora ya nishati.
Vilevile, Kamishna Luoga ametoa wito kwa Watanzania kutumia vifaa vyenye viwango vya ufanisi bora wa nishati ili kudhibiti upotevu wa umeme na kutumia gharama ndogo katika matumizi ya umeme.
Kwa upande wake, Naibu Balozi wa Ireland nchini, Mags Gaynor amesema Ubalozi huo unafurahishwa na jinsi Tanzania inavyotekeleza Programu ya Matumizi Bora ya Nishati ikiwemo kuandaa mkakati utakaopelekea Tanzania kutekeleza kwa ufanisi zaidi programu husika.
Akizungumzia Mkutano huo wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati, amesema ni hatua kubwa katika safari ya mabadiliko kuelekea kwenye matumizi bora ya nishati pamoja na kuwa njia ya kusukuma ajenda ya matumizi bora ya nishati.
Kwa upande wake, Programu Meneja wa Miradi ya Nishati kutoka EU, Massimiliano Pedretti ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa programu hiyo ambayo imeonesha mafanikio makubwa na kueleza kuwa Umoja huo utaongeza muda wa utekelezaji wa programu hiyo nchini ambayo ilikuwa ikifikia ukomo mwaka huu wa 2024 lakini sasa itaisha mwaka 2025 pamoja na kutanua wigo wa kazi pamoja na ufadhili.
Meneja wa Mradi wa masuala ya Nishati na mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Ulaya (EU), Massimiliano Pedretti akifafanua jambo wakati wa mkutano na Vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu Mkutano wa Kikanda wa Matumizi bora ya Nishati unaotarajiwa kufanyika Mkoni Arusha mapema mwezi Desemba .
Naye, Abbas Kitogo, Mtaalam wa Miradi kutoka UNDP, amesema Mkutano huo wa kikanda, utakuwa ni sehemu ya kubadilisha ujuzi, uelewa na kuhakikisha kunakuwa na uelekeo mmoja katika matumizi bora ya nishati kwani kila mmoja akifanya juhudi matumizi ya nishati yanatupungua na kuelekezwa kwenye sehemu zenye uhitaji na kupunguza gharama za nishati ambazo zinaweza kuelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.
Habari na Mwandishi wetu
Muhariri: Eunice Jacob.
0 Comments