Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Desemba 19, 2024 mkoani Kagera wakati akizungumza katika Tamasha la Pili la Uwekezaji la mkoa huo ikiwa sehemu ya Wiki ya Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani).
“Nawapongeza
waandaaji wa Kongamano hili na kama kuna watu wamekuja kuwekeza hapa napenda
kuwapongeza wale mlioitikia wito tangu kwenye kongamano la kwanza na kuja
kuwekeza hapa,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza
“Maombi yangu baada ya mkutano huu waje wengine kuwekeza na tutumie fursa hii
ya uwepo wa mkoa huu kijiografia na kutumia fursa zilizopo,”
Aidha,
amewaasa wananchi wa Mkoa wa Kagera
kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa na
kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.
Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Inocent Bashungwa akiongea na baadhi viongozi na wafanyabishara wa Mkoa wa Kagera
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa amesema chimbuko la Tamasha hilo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeta ifanyike tathmini ili kujua sababu za kudorora kwa uchumi na maendeleo ya Mkoa wa Kagera. Amesema mnamo mwaka 2022 wadau walikutana na kuainisha chanzo cha mkwamo kama mkoa.
“Wananchi
wa Kagera tuna bahati ya kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Rais Samia na
utashi wake wa kisiasa unasaidia mkoa wetu kutupa miradi mbalimbali ya
maendeleo na hivyo inatupa fursa zaidi ya kukuza uchumi wetu,” amesema Mhe.
Bashungwa.
Ameendelea
kueleza kuwa sababu za kijiografia kwa mkoa wa Kagera pia zinauweka katika
nafasi ya kimkakati kuleta maendeleo "Kijiografia tunamshukuru Mungu mkoa
wetu upo eneo la kimkakati na tuna rasilimali watu wa kutosha hivyo
tunawakumbusha wenzetu waliopo maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kukumbuka
nyumbani licha ya majukumu yao huko walipo,”
Mhe.
Bashungwa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi wa miradi mikubwa kama
vile ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi ambalo linatarajiwa kuzinduliwa mwezi
Februari 2025, ujenzi wa barabara na pamoja na kuzungumizia hitaji la mkoa wa
Kagera kuingia kwenye Gridi ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa akieleza mafanikio ya Tamasha la Ijuka Omuka wakati wa Kongamano la wafanyabiashara
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa amesema kuwa lengo la Tamasha hilo
la Pili la Uwekezaji la Mkoa wa Kagera ni kutoa fursa kwa Serikali na mrejesho
kwa wadau juu ya mafanikio na mipango ya Serikali kuhusu uchumi wa mkoa huo.
Akielezea
wasilisho lake la miradi na fursa zilizopo mkoani humo, ametaja baadhi ya
miradi inayoendelea kutekelezwa kuwa ni ujenzi wa barabara za kimkakati zenye
urefu wa km 265.4 zinazogharimu shilingi bilioni 340.49 na ujenzi wa madaraja
matano utakaogharimu shilingi bilioni 45.2.
Miradi
mingine ni vituo vinne vya umeme vilivyojengwa kwa shilingi bilioni 163.
Katika
sekta ya kilimo, Mhe. Mwassa amesema mkoa wake una mikataba miwili ya miradi ya
umwagiliaji inayogharimu shilingi bilioni 2.9.
Halikadhalika,
mkoa huo unatekeleza miradi mikubwa ya maji ya itakayogharimu kiasi cha
shilingi bilioni 191 na kunufaisha zaidi ya wananchi 500,000.
Ameendelea
kusema mkoa wake umepakana na nchi jirani nne na mikoa ya Kanda ya Ziwa
Victoria na hivyo kuwahakikishia soko la uhakika wa bidhaa.
Aidha,
amewapongeza wawekezaji mkoani humo kwa kujenga viwanda baada ya kuvutiwa na
fursa zilizopo mkoani humo.
Pia,
ametoa wito kwa wananchi kufuga samaki na dagaa katika vizimba na kuongeza
thamani ili waweze kuuza nje ya nchi badala ya sasa ambapo wanunuzi kutoka nje
ya nchi wananunua dagaa moja kwa moja kwa wafugaji wadogo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye picha ya pamoja na wabunge wa mkoa wa kagera wakati wa ufunguzi wa kongamano la Ijuka Omuka.
Mhe. Mwassa amehamasisha uwekezaji wa hoteli mkoani humo “Mikutano hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haifanyiki hapa Kagera kwa sababu hatuna uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu, mfano Polisi kutoka nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walipenda kuja hapa kufanyia mkutano wao haikuwezekana kwa sababu hatuna ukumbi wa kuhifadhi watu 3,000 kwa pamoja hivyo walienda mahali pengine” amebainisha Mhe. Mwassa.Vilevile,
Mhe. Mwassa ameonesha kiu yake ya kuona uwanja wa ndege wa Omukajunguti
ukijengwa na kukamilika ili kutoa huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa
uchumi wa mkoa huo.
Mhandisi
kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Emannuel
Mayanga amesema kuwa kupitia Miradi ya Kupendezesha Miji (TACTIC) Manispaa ya
Bukoba itanufaika na ujenzi wa barabara zenye urefu km 10.75, uwekaji wa zaidi
ya taa za barabarani zaidi 800 zitakazosaidia kuangaza Bukoba wakati wa usiku,
uboreshaji wa kingo za Mto Kanoni pamoja na uboreshaji wa soko.
Kupitia
tamasha hilo wadau na wawekezaji wamejadiliana kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji
zilizopo mkoani humo.
Na Mwandishi wetu.
Mhariri; Ramadhan Zaidy
0 Comments