Wabunge wa Ufaransa wamepiga kura ya kutokuwa na imani na
serikali, hatua ambayo imelitumbukiza taifa hilo katika mzozo mkubwa wa
kisiasa.
Wabunge wanaoelemea mrengo mkali wa kulia na wa kushoto
waliungana kuunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Michel
Barnier, kwa wingi wa kura 331.
Hatua hiyo inamlazimu
waziri mkuu huyo kukabidhi barua ya kujiuzulu pamoja na serikali yake kwa Rais
Emmanuel Macron,huku serikali hiyo ikiwa
imedumu madarakani kwa miezi mitatu pekee ikiwa ni miongoni, mwa zile
zilizokaa madarakani mwa muda mfupi zaidi tangu mwaka 1958.
Vyama vya mirengo ya kulia na kushoto vimemuondoa Barnier kwa kutumia madaraka yake maalum ya kikatiba kutekeleza
sehemu ya bajeti bila kupata idhini ya bunge.
Kabla ya kura
kupigwa, Barnier aliwaambia wabunge kwamba nakisi iliyopo isingeweza kuondoka
kwa hoja ya kumuondowa yeye madarakani, na kwamba serikali yoyote itakayokuja
baada yake itakumbwa na tatizo hilo la kukabiliana na nakisi ya bajeti.
Waziri Mkuu wa Ufaransa aliyeondoshwa kwa kura ya kutokuwa na imani, Michel Barnier.Rasimu ya bajeti hiyo
ilikuwa inataka euro bilioni 60 ili kuziba nakisi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kuangushwa kwa kura ya
kutokuwa na imani bungeni tangu mwaka 1962. Hatua hii, inatajwa kuchangiwa
na uamuzi wa Macron kuitisha uchaguzi wa mapema mwezi Juni mwaka huu,
ambapo matokeo yake yalikuwa ni bunge lililopasuka likiwa na wabunge wengi
kutoka upinzani.
Kutokana na kuporomoka kwa serikali hii, sasa Ufaransa
inaelekea kuumaliza mwaka huu bila serikali madhubuti wala bajeti ya mwaka
2025, ingawa katiba inaruhusu kuchukuliwa hatua maalum ambazo zitaepusha
kufungwa kabisa kwa shughuli za serikali kama ilivyo kwa Marekani.
Kwa upande mwengine, mpasuko wa kisiasa wa Ufaransa
utaudhoofisha zaidi Umoja wa Ulaya, ambao tayari unakabiliana na kuporomoka kwa
serikali ya mseto nchini Ujerumani,
Mhariri:Harieth Dominick.
0 Comments