Watoto hususani wanafunzi katika mkoa wa shinyanga wako katika hatari ya kupata utapiamlo na kusitisha masomo kutokana na ukosefu wa chakula cha kutosha kufuatia jamii mmoani humo kushindwa kuzalisha chakula cha kutosha kwa sababu za ukame.
Wakizungumza na waandishi wa habari
kutoka chama cha waandishi wa habari za vijijini nchini Tanzania (RUJAT) baadhi
ya wakulima wa kijiji cha Songambele, kata ya Salawe, wilaya ya Shinyanga
Vijijini, wanakabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hali
inayozidisha matishio ya kiusalama na hofu ya kutokea kwa baa la njaa na na
ongezeko la umasikini.
Wamebainisha kuwa mabadiliko ya
tabia nchi yamesababisha kubadilika kwa majira ya mvua na kupungua kwa mvua za
kutosha, kupungua kwa mavuno, na changamoto za maji ya umwagiliaji, hasa wakati
wa kiangazi.
Samwel Gulaka, mkazi wa kitongoji
cha Machongo, anaeleza jinsi mabadiliko haya yameathiri familia yake na
kupelekea watoto kuanza kuzorota kwenye mahudhurio shuleni na kuyumba kwa afya.
"Mimi ni mkulima wa bustani
kwa zaidi ya miaka kumi, kilimo hiki kimekuwa chanzo cha kipato changu lakini
tangu mwaka 2022, hali imekuwa mbaya ambapo Mwaka huo, mazao yangu yalinyauka
kwa sababu ya ukosefu wa maji ya kumwagilia nilitumia gharama kubwa lakini
sikuweza kupata mavuno kabisa hali hiyo ilisababisha njaa na matatizo makubwa
ya kifamilia," anasema Gulaka kwa masikitiko makubwa.
Gulaka anategemea kilimo cha
bustani kwa mahitaji yote ya familia, ikiwa ni pamoja na kununua chakula na
kusomesha watoto hata hivyo, kuanzia mwaka 2022, maji yamekuwa yakikauka kila
kiangazi, na hali hii imelazimisha baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao
fulani. "Tunaomba serikali na wadau wengine watujengee kisima cha maji au
malambo makubwa ambayo yatatuwezesha kupata maji ya uhakika wakati wote wa
Bustani," anaomba Gulaka.
"Kilimo cha bustani kimekuwa
changamoto Nyanya ambazo zamani nilikuwa napata milioni mbili kwa miche 2000,
sasa nalazimika kuishia na shilingi laki tano tu hali ya ukosefu wa maji wakati
wa kiangazi, kutoka Juni hadi Septemba, inaharibu mazao na kutufanya tupate
hasara kubwa," anasema.
Lutonja anasema changamoto hizo
zimemlazimu kufanya vibarua ili kulisha familia na kusomesha watoto.
"Kuna wakati nilishindwa
kabisa kusomesha mtoto wangu kwa sababu sikuwa na pesa baada ya mazao
kuharibika Kilimo cha bustani, ambacho kilikuwa cha faida kubwa, sasa
kinaonekana kuwa mzigo," anaeleza kwa uchungu.
Simon Mayala, mkulima wa mpunga na
mahindi kutoka kitongoji cha Kituli, anasema kuwa mvua zisizotabirika
zimepunguza mavuno kwa kiasi kikubwa. "Zamani nilikuwa napata gunia 30 kwa
hekari mbili za mpunga, lakini sasa napata gunia 10 tu. Mahindi, ambayo zamani
nilivuna gunia 20 kwa hekari mbili, sasa naishia na gunia tano mavuno haya
hayakidhi hata chakula cha familia, achilia mbali mahitaji mengine kama ada za
shule," anasema Mayala.
Shija Ntemi, mkulima mwingine wa
mahindi, anasema mwaka 2023 alipata gunia mbili tu kutoka hekari saba alizolima
hali hiyo ilimfanya abadilishe mazao na kulima mihogo, ambayo ilimletea gunia
28 hata hivyo, bado hajafikia malengo yake ya kuendesha familia na kusomesha
watoto saba. "Nikiwa na watoto watatu sekondari na wengine shule ya
msingi, najikuta nikikopa mara kwa mara ili kuhakikisha wanasoma Kilimo ndiyo
tegemeo letu, lakini hali ya mvua imekuwa tatizo kubwa," anasema Ntemi.
Hali hii imesababisha baadhi ya
wakulima kubadili mbinu na kuanza kutumia teknolojia za kisasa ambapo George
Lameck, mkulima wa kisasa wa mpunga na mahindi, anasema kuwa kilimo cha kisasa
kimekuwa na faida kubwa licha ya changamoto za tabianchi. "Mwaka 2023,
nililima hekari moja ya mpunga na kupata gunia 25 Kilimo cha kisasa
kinanisaidia kutumia mbegu za muda mfupi na kupata mavuno mengi," anasema
Lameck, akihimiza wakulima wengine kuachana na kilimo cha jadi.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha
Songambele, Bi. Evalina Isack, anasisitiza umuhimu wa kilimo cha kisasa.
"Mabadiliko haya ya tabianchi yamekuwa yakiwaathiri sana wakulima
wanaotegemea kilimo cha jadi.
Nawashauri wakulima kutumia
pembejeo za kisasa ili kuongeza mavuno na kukabiliana na hali ya hewa isiyotabirika,"
anasema Evalina.
Kwa upande wake, Afisa kilimo wa
kijiji hicho anashauri wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame kama mtama,
alizeti, viazi, na mihogo ili kupunguza athari za moja kwa moja za mabadiliko
ya tabianchi.
Kupitia msaada wa serikali,
mashirika, na wadau wengine, wakulima wa Songambele wanaweza kupunguza
changamoto wanazokabiliana nazo na kujenga maisha bora kwa familia zao.
Miongoni mwa Mashirika yanayojihusisha
na utoaji wa elimu kuhusu masuala ya kilimo endelevu na kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabia nchi ni Chama cha waandishi wa habari za Vijijini (RUJAT),
Shirika la We-World la nchini Italia, shirika la mpango wa chakula la Umoja wa
mataifa (WFP) shirika la kilimo na chakula duniani (FAO) pamoja na Wizara
mtambuka za serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania hususani Kilimo, Afya,
Mazingira, Mifugo na Umwaguliaji.
Mwandishi: Misalaba Mapuli
Mhariri: Prosper Kwigize
0 Comments