Mkurugenzi Wilaya ya Kasulu ashiriki zoezi la Usafi wa Mazingira Miaka 63 ya Uhuru

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Semistatus  Mashimba leo Desemba 9. 2024, ameongoza zoezi usafi katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu na vituo vyote vinavyotoa huduma za afya lililoambatana na uchangiaji wa damu kwa kushirikiana na Kambi ya Jeshi ya 825 Mtabila.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Usafi na Udhibiti wa Taka wa Halmashauri hiyo, Ndelekwa Vanica amehimiza jamii kushiriki mazoezi ya usafi ya kitaifa likiwemo lile la kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili mazingira yawe safi.

“Serikali imeshatoa tamko kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki shughuli za usafi, na niwaombe Kambi ya mtabila kila tutakapowaita katika mazoezi hayo mje kama njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kushiriki usafi huo” amesema.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mageni Pondamali ameishukuru Kambi ya JKT Mtabila kwa kuchangia damu kutokana na hospitali hiyo kuwa na uhaba wa huduma uliokuwepo hospitalini hapo.

 Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Maabara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Jasimen Meru amesema zoezi la uchangiaji damu limesaidia ukusanywaji wa chupa 36 zenye ujazo wa 'Mils' 450 ambapo damu hiyo itaokoa maisha ya watu wenye matatizo ya Seli Mundu,wamama wajawazito,watoto chini ya miaka mitano pamoja na majeruhi wa ajali.

Na mwandishi wetu.

Post a Comment

0 Comments