Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ACT Wazalendo Abdul Nondo amepatikana

Mwenyekiti wa Ngome ya vijana wa ACT Wazalendo Abdul Omary Nondo amepatikana usiku wa kuamkia leo katika fukwe za Coco beach zilizopo katika bahari ya Hindi jijini Dar es salaam. 

Akitoa taarifa hiyo usiku huo Makamo Mwenyekiti Bara wa chama cha ACT Wazalendo Isihaka Mchinjata amesema Abdul Nondo alitupwa katika fukwe hizo na kusaidiwa na wasamaria wema ambao walimpeleka katika ofisi za cha cha ACT Wazalendo zilizopo Kinondoni jijini Dar es salaam. 

Mchinjata amesema hali ya Abdul Nondo ni mbaya kwasababu amepigwa sana katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

 Amesema kwa sasa bado hawana taarifa zaidi juu ya tukio hilo japo mhanga amepatikana lakini kutokana na hali aliyokutwa nayo hajaweza kujieleza zaidi.

 “Hatua ya kwanza ni kuangali hali aliyonayo hivyo tukalazimika kumuwahisha hospitali ya Agakhan kwa ajli ya kupatiwa matibabu, maana alikuwa na maumivu makali karibia mwili mzima,” amesema Mchinjati.

 Aidha ameeleza namna ambavyo taarifa ziliwafikia kuwa ni baada ya kupigiwa simu na watu waliokuwepo wakati wa tukio majira ya asubuhi katika Stendi ya mabasi ya Magufuli baada ya kuokota begi lenye nguo za ACT Wazalendo.

 “Tukio lilipotokea watu walioshuhudia kurupushani wakati wa utekeji waliokota begi lenye nguo za ACT Wazalendo ndipo wakampigia simu John Mnyika na ufuatiliaji ukaanza haraka uzuri namba za gari lililotumika zilipatikana,” amesema Mchinjata.

 Abdul Nondo ni Mwenyekiti wa Ngome ya vijana wa ACT Wazalendo jana alitekwa na watu wasiojulikana baada ya kushuka kwenye basi akitokea mkoani Kigoma, tukio hilo ni muendelezo wa matukio ya utekaji yanayoendelea hapa nchini kwa siku za hivi karibuni.

Muandishi: Mussa Mkilanya.

 

Post a Comment

0 Comments