Nchi za EAC na SADC zimeazimia kuendeleza Teknolojia za Matumizi Bora ya Nishati

 


Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati uliohusisha Nchi 
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika jana jijini Arusha umetoka na maazimio mbalimbali yatakayowezesha nchi za EAC na SADC kuwa na Matumizi Bora ya Nishati.

Moja ya maazimio hayo ni kuendeleza Teknolojia za Matumizi bora ya Nishati ili kuwa na ufanisi katika matumizi ya nishati hiyo.

 Mkutano huo uliokuwa ukifanyika jijini Arusha Disemba 4-5 mwaka huu umefungwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo ambaye ameeleza kuwa umehusisha  Watunga Sera, Sheria, Viongozi, Wataalam na Wabobezi katika masuala ya Nishati kwa lengo moja la kuwa na matumizi sahihi ya Nishati.

Dkt. Jafo amesema lengo la nchi ni kuendelea kukuza uchumi, viwanda vifanye kazi na biashara zifanyike kwa ufanisi lakini hilo litawezekana ikiwa kuna nishati ya kutosha ambayo uwepo wake unategemea usahihi katika matumizi yake.

Ameeleza kuwa, Tanzania inatilia mkazo suala la matumizi bora ya
nishati ambapo kwa sasa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango fanisi vya vifaa vya nishati vinavyozalishwa au kuingizwa nchi ambavyo vitawezesha nchi kutumia umeme kwa ufanisi.

Amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya Nishati  ambapo uwekezaji huo amesema kwamba una maana kubwa  katika kuendeleza viwanda na biashara.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani  Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Nishati, wakati akifunga Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati uliofanyika Arusha.

Aidha, ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kuratibu Mkutano huo wa Siku mbili kwa kushirikiana  na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati imejipanga kutekeleza Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati uliozinduliwa tarehe 4 Desemba 2024  kwa kuhakikisha Mkakati huo unatekelezwa kwa kuwekewa bajeti ili nchi iweze kuwa na ufanisi katika vifaa vya nishati.

Amesema kupitia Mkutano wa REEC 2024 maazimio mbalimbali yamefikiwa ikiwemo kufanya tafiti za pamoja ili kuboresha matumizi bora ya nishati na kuihusisha kikamilifu Sekta Binafsi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu, Mhe.Selemani Kakoso amsipongeza Serikali kwa kuendesha na kusimamia mkutano wa REEC 2024 ulioleta mafanikio makubwa  ikiwemo mafunzo na kubadilishana uzoefu ili kuwa na ufanisi.kwenye matumizi ya nishati.


Mwandishi: Na Mwandishi wetu.




Post a Comment

0 Comments