Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
kuchukua hatua mara moja kwa kuwaandikia timu ya Simba SC na kuwanakili
Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) kugharamikia uharibifu uliotokea katika uwanja wa Benjamin Mkapa wakati mechi ya Kombe la
Shirikisho barani Afrika kati Simba SC dhidi ya SC Sfaxien ya Tunisia zilipwe.
Taarifa hiyo imetolewa Leo na kitengo cha mawasiliano Serikali kupitia
wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo imeeleza kuwa wizara imesikitishwa
na vitendo vya mashabiki kung’oa na kuharibu viti katika Uwanja wa Benjamin
Mkapa, jijini Dar es Salaam katika mchezo huo ambao ulipigwa jana Desemba 15,
2024.
Aidha Prof.Kabudi amewataka mashabiki
wanaoingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa
uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.
"Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubariki
na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja
na kuwaandikia Simba Sports Club na TFF, wapeni ushirikiano Polisi ili watu
wote waliokuwa wanang'oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za
kisheria, lazima tabia hii ikomeshwe" amesema Prof. Kabudi.
Baadhi ya mashabiki wakifanya uharibifu katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi
Kanda Maalum Dar es Salaam limethibitisha kutokea kwa fujo katika uwanja wa
benjamini mara baada ya mchezo huo kutamatika kwa Simba SC kuibuka na ushindi
wa mabao 2-1 dhidi CS Sfaxien ya Tunisia.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es
Salaam,Jumanne Muliro Jumanne, amesema
fujo hizo zilitokana na mashabiki wa CS Sfaxien kutoridhika na maamuzi ya Refa,
ambaye aliongeza dakika 7 kufidia dakika zilizopotea, hatua hiyo ilipelekea
Simba SC kupata goli la pili la ushindi.
"Wachezaji wa CS Sfaxien na benchi lao walimfuata Muamuzi na kuanza
kumshambulia hali iliyochochea mashabiki wao kufanya uharibifu," Amisema
Kamanda Muliro.
Hata hivyo Muliro amebainisha kuwa Shabiki
mmoja wa CS Sfaxien ameumia katika vurugu hizo na kupatiwa huduma ya kwanza na
jumla ya viti 256 ikiwa viti 156 vya
bluu na 100 vya orange vimeripotiwa kung’olewa na mashabiki wa timu hiyo.
Jeshi la Polisi limeahidi kushirikiana na
mamlaka za soka kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivyo visivyokubalika.
Taarifa kutoka Wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Taarifa kutoka jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar Es Salaam
Mwandishi; Sharfat Shinji
Mhariri; Ramadhani Zaidy
0 Comments