Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara Nchini.


 Serikali imesema itaendeleza jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa lengo la kuboresha shughuli za biashara, uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi Mwaka huu na Mkutano Mkuu wa 49 wa Mwaka 2024 wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA). 

Dkt. Biteko ameeleza umuhimu wa sekta binafsi na kusema kuwa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla inakisiwa kuwa vijana zaidi ya bilioni 12 wanaingia katika soko la ajira na kati yao asilimia 70 wanategemea sekta binafsi ndio maana Serikali imeendelea kushirikiana na kutatua changamoto za sekta binafsi. 

“Hivi karibuni mlitoa malalamiko kadhaa ikiwemo ya kukwamisha shughuli za biashara na Serikali imeyatatua kwa kushirikiana nanyi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko. 

Ametaja baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kuwa ni pamoja na kufanywa marekebisho ya sheria na kanuni 55 na sheria zingine 16 na kanuni zake zinaendelea kufanyiwa kazi. 

“Serikali imeondoa mwingiliano wa majukumu na kuanzisha mamlaka mfano sasa tuna Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kurahisisha shughuli zenu. Pia, imepunguza idadi ya muda wa kupata huduma kutoka siku 14 hadi tatu na kutoka siku saba hadi tatu za kusafirisha mizigo kutoka Dar es salaam hadi Tunduma,” amesema Dkt Biteko. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. John Lukuvi.


Pamoja na hayo Dkt. Biteko amefafanua kuwa Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA) imepunguza tozo 16 za biashara ambazo kupitia hizo Serikali inapoteza mapato kiasi cha shilingi bilioni 37 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha mazingira ya biashara nchini. 

Pia amezungumzia viashiria vya ukuaji wa uchumi na kusema kuwa kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme ambapo awali hayakuwahi kuzidi megawati 219 kwa mwaka na kuwa mwaka 2024 mahitaji ni megawati 420. 

“Mkifanyabiashara maana yake mahitaji ya nishati ya umeme yanaongezeka na hii ni kwa sababu viwanda vingi vimejengwa na uchumi unachangamka. Tunaanza kuona wananchi wanatumia umeme megawati 52 na viwanda vinatumia megawati 48 hii ni kiashiria kuwa uchumi unaendelea kukua vizuri,” amebainisha Dkt. Biteko. 

Vilevile, amewaasa wafanyabiashara nchini kulipa kodi kwa hiari ili Serikali iweze kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali itakayosaidia utoaji huduma za kijamii kwa wananchi na kuchochea maendeleo huku akiwataka kuzalisha malighafi na bidhaa zenye ubora zitakazovutia masoko na kutoa ajira kwa watu. 

“Nchi yetu tutaijenga wenyewe na tuambiane ukweli kwamba kulipa kodi ni wajibu wetu, kwa mikataba hii iliyowekwa saini hapa leo TCCIA muwe mawakala wa kutoa elimu ya mlipa kodi kwa wananchi ili watu waone heshima ya kulipa kodi,” amesema Dkt. Biteko. 

Wadau wa uwekezaji kutoka Serikalini na Sekta binafsi wakiwa katika Kongamano la Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji.

Ameendelea kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini huku akivitaka vyama vya kisekta kuepuka migogoro na kusisitiza upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwao. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. John Lukuvi amesema kusanyiko hilo la zaidi ya wafanyabiashara na wakulima 300 kutoka nchi nzima ni muhimu na kuwa kupitia jukwaa hilo Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kukuza sekta binafsi nchini. 

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo amesema kuwa Mkoa huo umekuwa na ushirikiano mzuri na TCCIA katika shughuli mbalimbali. 

Mwandishi: Na Mwandishi wetu.

Post a Comment

0 Comments