Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nkasi, Afraha
Hassan amesema wanafunzi waliofukuzwa shule kwa madai kuwa wazazi wao ni
wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wamerudishwa shuleni.
Akitoa taarifa hiyo leo Mkurugenzi huyo amesema
wanafuzi waliokutwa na Mkasa huo walikuwa tisa na tayari wamewarudisha muda
mfupi tangu taarifa ya kufukuzwa kwa wanafunzi hao wa Shule ya Msingi Izinga kusambaa
mitandaoni.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo ya Mkurugenzi imesema
wamebaini kuwa Mwalimu Mkuu aliwasimamisha shule wanafunzi hao na kuwataka
wazazi watafute shule nyingine na siyo kufukuzwa shule kama ilivyoripotiwa
katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Uamuzi wa kuwasimamisha wanafunzi hao haukufuata
utaratibu wa miongozo ya wizara. Aidha wanafunzi waliosimamishwa shule hawakuwa
na kosa lolote la kinidhamu,” amesema Mkurugenzi.
Aidha Mkurugenzi amesema hatua za kiutawala na uongozi
dhidi ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo zitachukuliwa pindi uchunguzi unaoendelea
utapokamilika.
Mapema leo asubuhi, Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliagiza timu ya wataalamu udhibiti ubora
kwenda kuchunguza taarifa ya wanafunzi hao wa Shule ya Msingi Izinga, iliyopo
Nkasi Kusini kufukuzwa shule kwa madai ya wazazi wao kuipigia kura CHADEMA
katika uchaguzi wa serikali za mitaaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Muandishi: Mussa Mkilanya.
0 Comments