Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na
uendeshaji wa UDSM Marathon na kusema kuwa inasaidia kufanikisha malengo ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya kuendelea kutoa elimu bora na kuboresha
mazingira ya wanafunzi.
Dkt. Biteko amesema
hayo leo mara baada ya kushiriki mbio hizo za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM MARATHON) zilizofanyika chuoni hapo.
“Ni dhahiri kwamba
mbio hizi zimekuwa muhimu kwa Chuo hiki na jamii kwa ujumla. Tukio hili
limeleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi
za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Natambua
kwa misimu mitano mbio hizi zimekua zikichangia katika ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi
kinachojengwa hapa katika Kampasi Kuu ya Mwalimu Nyerere Mlimani. Ujenzi wa
kituo hiki ulianza kwa michango kutoka kwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na washirika mbalimbali wa maendeleo ya elimu ambapo jumla ya shilingi
bilioni 4.4 zimechangwa kutoka kwa wadau.”
Aidha, awamu ya
kwanza ya ujenzi imekamilishwa kwa kutumia fedha za ndani na hivyo kazi
kubwa iliyobaki ni kukamilisha awamu ya pili ili kutimiza ndoto ya kuwa na
Kituo cha Wanafunzi kitakachowezesha wanachuo kuwa na maeneo ya
kujifunzia na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Ujenzi wa awamu ya
pili unahitaji shilingi bilioni 3.3 na hivyo kufanya gharama za ujenzi kwa
awamu hiyo kufikia shilingi bilioni 9.4 badala ya shilingi bilioni 6
zilizokadiriwa awali ambazo zimebadilika kwa sababu mbalimbali.
Naibu Waziri Mkuu Mhe.Dotto Biteko pamoja na Rais wa awamu ya nne Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa UDSM Marathon.
Akiwahakikishia
ushiriki wake katika kufanikisha ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo Dkt. Biteko
amesema “Nataka niwatoe wasiwasi kuwa jambo hili ni letu sote kwa kuwa majengo
haya yatatumika kwetu sote. Nalibeba suala hili kwa uzito wake ili
kilichoahidiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi kipatikane kwa wakati,”
Pia, ametoa wito kwa
wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada za kuwezesha mbio hizo kufanyika kwa
ustadi mkubwa na kwa kuwa zimeonesha kupitia mshikamano, wanaweza kufanikisha
malengo makubwa ya kijamii na kielimu. Sambamba na kuhimiza uongozi wa Chuo
kuandaa namna ya kukutanisha wadau zaidi ili kuchangia fedha za kukamilisha
ujenzi wa kituo.
Vilevile, Dkt.
Biteko amempongeza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Awamu ya Nne
Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa usimamizi wake katika shughuli za maendeleo
ya Chuo hicho.
Kwa upenda wake,
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amesema kuwa Chuo hicho kinathamini mchango wa Serikali katika ujenzi
wa Kituo hicho cha wanafunzi.
Naibu Makamu
Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (Utawala na Fedha), Prof. Bernadeta Kilian
amesema Chuo hicho kilianzisha ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya
kupumzika na kukuza uwezo wa kubuni au kupata mawazo Mapya.
Mwandishi: Na Mwandishi wetu.
0 Comments