MKUU wa Wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba amesema zoezi la
kuwalipa fidia wananchi wa kijiji cha Ngombo kilichopo ndani ya Pori la Akiba
Kilombero mkoani Morogoro linaendelea vizuri.
Amesema 93% ya wananchi wote wamekwishalipwa fidia zao kwa
ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo na 7% ya wananchi
waliosalia wanaendelea kushughulikiwa kukamilisha malipo yao.
Akizungumzia zoezi hilo Desemba 31, 2024 wilayani humo, Sebastian
amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh billioni 6.9 kulipa wananchi 1,056
ili waweze kuhama kwa hiari kutoka maeneo ya hifadhi huku akitoa maelekezo kwa
watendaji wa vijiji 32 wilayani Malinyi kuwapokea ili waweze kuendelea na
shughuli zao za kila siku.
Kuhusu wanafunzi waliokuwa wanasoma shule katika kijiji cha
Ngombo, mkuu huyo wa wilaya amesema amekwishatoa maelekezo kwa ofisa
elimu kuwapokea na kuwasajili katika shule zilizopo kwenye vijiji vilivyo ndani
ya wilaya hiyo bila masharti yoyote ili waweze kusoma kwa uhuru.
Aidha, Sebastian amesema wananchi wa kijiji cha Ngombo
waliandaliwa mapema kwa kupewa elimu juu ya malipo ya fidia ili weweze kuhama
kutoka katika eneo la Hifadhi ya Kilombero tangu mwezi Agosti, 2024.
Hivyo, walikuwa na uelewa kuhusu zoezi hilo na amewataka
kuepuka watu wenye nia ovu ya kupotosha dhamira njema ya zoezi hilo.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Biro, Elizabeth Mnenuka amekiri kupokea zaidi ya wananchi 50 katika Kijiji cha Biro na wengine zaidi ya 30 katika kijiji cha Mbalinyi na kuongeza kuwa baadhi yao tayari wameshapatiwa maeneo kwa ajili ya kuendeleza kwa kilimo na makazi
Nao wananchi waliohamia kijiji cha Biro kutoka kijiji cha Ngombo wameishukuru Serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, Rais kwa kuwalipa fidia zao Kwa wakati ambazo zimewasaidia kuhama na kuanza maisha mapya katika vijiji jirani.
“Toka nitoke Kijiji cha Ngombo ambapo tuliondolewa kisheria
kwakweli sina changamoto yoyote kimaisha, niko vizuri naishi vizuri na familia.
Naishukuru Serikali, fidia nimepata kwahiyo mpaka hapa sina neno na Serikali”
amesema Daudi Deodatus Lyambu aliyekuwa mkazi wa Ngombo ambaye sasa amehamia
kijiji cha Biro.
mnamo Februari 17, 2023 Pori la Akiba Kilombero lenye sehemu
A na B lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 64 kufuatia kupandishwa hadhi
kwa sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero kuwa Pori la Akiba.
Aidha, kufuatia kuanzishwa kwa Pori la Akiba Kilombero, masharti na sheria zinazosimamia eneo hilo zilibadilika ambapo shughuli zote za kibinadamu zimesitishwa isipokuwa zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria. Lengo la Serikali likiwa ni kuimarisha usimamizi wa eneo hilo kwa kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori ili kuongeza tija ikiwemo upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Mwl. Nyerere.
NA Mwandishi wetu
MHARIRI :Abel Mahenge .
0 Comments