Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa wahasibu barani Afrika kuisimamia taaluma yao
kikamilifu ili kuendeleza umuhimu na mchango na ukuaji wa uchumi duniani.Ameyasema hayo Desemba 04, 2024 wakati
akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika ufungaji wa Mkutano wa Pili wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi
za Afrika (AAAG) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha
(AICC).
“Nataka niwaombe wahasibu mtambue kuwa
taaluma yenu ni muhimu hata chochote kinachotokea katika sehemu zenu za kazi
mtalaumiwa, hivyo mzuie hasara zinazoweza kutokea," amesema Dkt. Biteko.
Amewaasa
kusimamia taaluma yao kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma hata kama
uamuzi wao unaweza kuwa na gharama“ Isimamieni taaluma yenu kwa wivu mkubwa na
kusema ukweli hata kama mtachukiwa, mahali pa kazi ili kuwe na ufanisi ni
muhimu kuwaheshimu wahasibu ili wakupe matokeo tarajiwa,”
Aidha, Dkt. Biteko amesema ni muhimu kwa
wahasibu hao kujiongezea ujuzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Pamoja na hayo amesema wahasibu
wanatakiwa kuwa washauri wazuri wa viongozi wao ili waweze kufanya maamuzi sahihi,
huku akisema AU inategemea wataalamu hao ili kuisaidia Afrika kunufaika na
rasilimali zake.
“AU inawategemea nyie wimbo wa Afrika ni
tajiri utabaki kwenye vitabu kama hatutachukua hatua,” amesema Dkt. Biteko.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande
amempongeza Mwenyekiti wa AAAG na Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Tanzania kwa
kuandaa mkutano mzuri na kuwataka wahasibu kuzingatia maadili ya kazi yao.
“Afrika tuna utajiri wa kuwa na watu
wenye uwezo mkubwa katika kada hii ya uhasibu na ni imani yangu kupitia mkutano
huu utaleta mabadiliko katika nchi zetu,” amesema Mhe. Chande.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akitoa hotuba ya kufunga Mkutano wa Pili wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi za Afrika (AAAG) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu
wa Nchi za Afrika ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Lesotho,
Malehlohonolo Mahase amesema kuwa Afrika inabadilika katika masula ya uhasibu
na kupitia mkutano huo wamepata fursa ya kubadilishana mawazo na ujuzi.
Amesema AAAG ni bodi ya kiafrika
inayolenga kwenda sambamba na Umoja wa Afrika huku ikisimamia nguzo za Umoja
huo na kuwa mikataba inayoridhiwa na AU inatekelezwa pia na AAAG ili kuwa na
ukuaji endelevu kwa nchi wanachama na Afrika kwa ujumla.
“Kipaumbele chetu kimekuwa ni wahasibu
wanavyoweza kusimamia masula ya uhasibu ikiwemo hazina za nchi zetu,
tumezungumzia kada ya uhasibu, kuimarisha mifumo yetu fedha na kushughulukia
upotevu wa fedha katika nchi zetu,” amesema Mahase.
Mahase amewataka Wahasibu Wakuu na
Wahasibu Afrika kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika taaluma yao
sambamba na kujiongezea ujuzi ili kuwa na ufanisi katika kazi zao.
Ametaja umuhimu wa wataalamu hao na
kusema kuwa Afrika inawahitaji zaidi wakati huu ili kukusanya mapato na kuzuia
njia zisizo halali za mianya ya fedha.
Akizungumzia baadhi ya maazio ya mkutano
huo “Mkutano huu umeazimia kuwa na matumizi bora ya rasilimali, kutumia mifumo
ya kihasibu inayoshabihiana, kuwa mafunzo ya mara kwa mara kwa watu wa kada ya
uhasibu,”
Amesisitiza “Kuongeza ushiriki wa
wananchi kuhusu bajeti katika utekelezaji na utoaji taarifa ili kuongeza uwazi
sambamba na kuwekeza kwenye masuala ya usalama mtandaoni,”
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wahasibu
Wakuu wa Nchi za Afrika, Fredrick Riaga ameipongeza Tanzania kwa kuhakikisha
mkutano huo unafanyika kwa mafanikio makubwa.
Amewashukuru Wahasibu Wakuu kutoka nchi
mbalimbali walioshiriki akisema ni kiashiria cha kuimarisha sekta ya uhasibu
Afrika ambapo washiriki 800 wametoka Tanzania huku mkutano wote ukiwa na idadi
ya washiriki 1,000 ambapo zaidi ya washiriki 1500 wamehudhuria mkutano huo
kutoka nchi 26 barani Afrika.
Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Tanzania,
Leonard Mkude amewasihi washiriki wa mkutano huo kufanyia kazi yote
waliyojifunza ili kuboresha kazi za uhasibu katika nchi zao.
Na Mwandishi wetu
0 Comments