Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof Palamagamba John Kabudi Disemba 04 Mwaka huu amekutana na kufanya kikao na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Mhe. Jaji Imani Aboud aliyeambatana na ujumbe kutoka Mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika
ukumbi wa Wizara Mtumba, jijini Dodoma viongozi hao wamejadili kuhusu nafasi ya
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu katika kusimamia na
kulinda Haki za Binadamu na Watu wa Afrika.
Waziri Kabudi amesema yapo maeneo ambayo
yanahitaji kuboreshwa zaidi katika Mahakama ili kuimarisha mahusiano mazuri
yaliyopo ambapo pia wamejadili changamoto zinazoikabili sekta ya Mahakama
ambapo wamekubaliana kuendeleza majadiliano kwa ajili ya kuzifanyia kazi
changamoto hizo ili kuiwezesha Mahakama kutimiza majukumu yake ambayo imepewa
chini ya Mkataba wa kuanzishwa kwa Mahakama hiyo.
Sambamba na hilo maeneo mengi ya majadiliano ni
pamoja na kuimarisha ushirikiano katika eneo la Rasilimali Watu ili kuwajengea
uwezo Maafisa wa Mahakama kwa kupata mafunzo na uzoefu katika Mahakama hiyo ili
Tanzania iweze kutoa mchango wake katika utekelezaji wa kazi za Mahakama hiyo.
Viongozi hao pia wamepitia mambo ambayo Tanzania
inawajibu wa kuyatekeleza chini ya Mkataba wa kuwa Mwenyeji wa Mahakama
hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Kabudi Kabudi
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo kubwa la
Mahakama Afrika, ambapo amesema kuwa mambo mengi yanayofanywa katika Mahakama
hiyo yanaendana na utekelezaji wa falsafa ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni Maridhiano,
Ustahimilivu, Kuboresha na Kujenga upya.
Waziri Kabudi amesema kuwa kwa sasa Wizara
inaandaa Muswada wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na katika
kufanya hivyo miongoni mwa nyaraka zitakazotumika ni pamoja na maamuzi ya
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Muandishi: Na Muandishi wetu.
0 Comments