Wizara ya katiba na sheria, TLS kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa nchini



Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema kuwa serikali imeingia makubaliano na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuwa na kambi maalumu ya mawakili watakaotembelea magereza yote nchini kwa lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa.

Makubaliano hayo yamefanyika Desemba 15 wakati Dk Ndumbaro akisikiliza matatizo na kuzungumza na wafungwa katika Gereza la Kiberege lililipo wilayani Kilombero mkoani Morogoro kupitia Kampeni ya ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’.

Waziri Ndumbaro ameagiza kambi hiyo ianzie kazi mara moja katika Gereza la Kiberege, ambapo mawakili wa TLS watashiriki kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa wenye changamoto mbalimbali za kisheria.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Damas Ndumbaro akitembelea wafungwa katika gereza la KKiberege, Morogoro 

Wakati wa zoezi hilo, Waziri Dk Ndumbaro ametoa  msaada wa kisheria kwa wafungwa 15 na mahabusu wawili  na amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha haki inapatikana kwa wafungwa na mahabusu wote, hususan wale waliofungwa kwa makosa ya kusingiziwa.

Kwa upande baadhi ya wafungwa katika gereza la Kiberege mkoani Morogoro wameeleza kufurahishwa na utaratibu na kampeni hiyo ya ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ ambayo utawasaidia kutambua haki zao za kimsingi kwa mujibu wa katiba na sheria.


Kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla. Utekelezaji wa kampeni unafanyika kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni na Wadau wa Maendeleo. 

Huku Lengo kuu la Kampeni ni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.

Mwandishi: Ramadhani Zaidy


Post a Comment

0 Comments