Takriban wakimbizi 10,000 wa DRC wamekimbilia nchini Burundi

Hizi ni takwimu za kuanzia Februari 14, 2025 hadi Februari 16 mwaka huu, ambapo zaidi ya Wakongo 10,000 waliokuwa wakikimbia mapigano mashariki mwa nchi hiyo waliingia Burundi, wakivuka mipaka ya Gatumba na Rusizi katika mikoa ya Bujumbura na Bujumbura.

 Hayo yametangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Martin Niteretse katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mapema leo jijini Bujumbura kufuatia kuongezeka kwa wakimbizi kutoka DRC wanaoingia nchini Burundi

Mh. Martin Niteretse Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Burundi, akizungumza na waandishi wa habari. Picha na. David Ndereyimana

Waziri Martin Niteretse alisema: “Watu hawa wanaundwa na makundi mbalimbali, kwahio tumeamua  kuwakusanya pamoja katika majimbo ya Bubanza na Cibitoke na maeneo mengine, mfano viwanja vya mpira na sehemu na sehemu  nyinginezo"

Mh. Niteretse amebainisha kuwa lengo la kuwaweka katika vituo maalumu vya mapokezi ni kutaka kujua undani wao na kuwabaini askari, raia na watu wengine wenye magonjwa mbalimbali na mahitaji maalum kama vile wajawazito na wengine wanaohitaji msaada wa haraka.

Imeelezwa kuwa shughuli za kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi hao zinaungwa mkono na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).

 Aidha Waziri huyo wa mambo ya ndani amefahamisha kuwa kazi hii inaenda sambamba na operesheni nyingine ambayo polisi wa Burundi wanaifanya katika wilaya mbalimbali, kwa ajili ya kuwabaini wageni nchini Burundi ambapo takriban watu 80 wamebainika kutokidhi masharti ya kuishi nchini Burundi na kufukuzwa.

Duru za kimataifa zinaweka bayana kuwa tayari waasi wa M23 wanaotajwa kuungwa mkono na Jeshi la Rwanda wanaendelea kuteka maeneo zaidi ya Congo mashariki baada ya kuukalia mji wa Goma kwa zaidi ya wiki moja.

Ripoti zinadhihirisha kuwa tayari Mji wa Bukavu uko chini ya himaya ya M23 na miji midogo kama vile Beni, Baraka na Uvira inanyemelewa na wapiganaji na jamii imeanza kuyakimbia makazi yao.

Mwandishi: David Ndereyimana, Bujumbura

Mhariri: Prosper Kwigize

Post a Comment

0 Comments