Dkt.
Biteko ameyasema hayo leo Februari 28, 2025 ofisini kwake Jijini Dar es salaam
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud
Hilal Al Shidhani.
“Mhe.
Balozi tunakushukuru kwa namna tunavyoshirikiana na uwepo wako nchini
umeendelea kuimarisha mahusiano na Serikali yako. Tunafurahia kuwa na uhusiano
huu wa kidiplomasia. Sisi tunaichukulia Oman kama marafiki na Mhe. Rais Samia
anapenda ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zingine, kanuni inayosema
ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako ni muhimu sana, amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea
kusema kuwa uwepo wa idadi kubwa ya Watanzania wanaofanya kazi nchini Oman ni
tafsiri ya urafiki na ushirikiano uliopo
baina ya nchi hizo.
Dkt.
Biteko amesema kuwa Tanzania itapeleka timu ya wataalamu nchini humo ili kujifunza
kuhusu masuala ya gesi. Pia, amemweleza Mhe. Balozi Al Shidhani kuhusu nia ya
Serikali ya kufanya mnada wa tano wa vitalu vya gesi kupitia Kongamano la
Mkutano wa 11 wa Afrika Mashariki wa Petroli kuanzia Machi 5 - 7 mwaka huu,
hivyo mnada huo ni fursa kwa kampuni za kutoka nchini Oman kuwekeza nchini.
Aidha,
fursa zingine zinazotokana na ushirikiano huo ni kuendeleza ufadhili wa masomo
kwa vijana wa Tanzania kwa ajili ya
kusoma nchini Oman hususan katika masuala ya biashara, mafuta na gesi.
“Ushirikiano
wetu wa Wizara ya Nishati na Serikali ya
Oman haukwepeki katika mnyororo mzima kuanzia uzalishaji hadi katika biashara.
Tupo kwenye njia sahihi na tunaamini katika ushirikiano huu tutapiga hatua
zaidi na tutaacha alama,” amesema Dkt. Biteko
Akizungumzia
kuhusu ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia amesema kuwa nchi za
Afrika na nchi zinazoendelea zizungumze lugha moja kuhusu namna ya kuzalisha
nishati kwa ajili ya kusaidia watu milioni 600 wanaokosa nishati Barani Afrika
kwa kutumia rasilimali zilizopo huku akitolea mfano baadhi ya nchi zilizondelea
kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha umeme lakini kutoruhusu nchi za
Afrika kufanya hivyo.
“Afrika
hatufanyi uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa kama nchi zilizoendelea na pia kama
kuna teknolojia wanayoweza kutupa basi itumike ili kupunguza uchafuzi wa hali
ya hewa, lakini kiwango cha uchafuzi
hakifanani kati ya nchi hizi hivyo masharti kuhusu kupunguza uzalishaji wa hewa
ukaa hayapaswi kuwa sawa kwa wote. Hivyo tunahitaji kuzungumza lugha moja na
nimeona baadhi ya nchi za Bara la Asia zinazungumza lugha moja katika hili,”
amesisitiza Dkt. Biteko.
Pia,
amezipongeza Kampuni za nchini Oman
zinazofanya biashara Tanzania kwa kuendelea kufanya shughuli zao kwa
ufanisi pamoja na kuzikaribisha kuwekeza katika sekta ya gesi kwa kuwa nchi ina
kiwango kikubwa cha gesi baada ya kuhamia katika uzalishaji wa umeme kwa
kutumia maji.
Kwa
upande wake, Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud Hilal Al Shidhani amesema kuwa
nchi yake inafurahia uhusiano uliopo kati yake na Tanzania na wanajivunia kuwa
na watu zaidi ya asilimia 30 wanazungumza lugha ya Kiswahili kati ya watu
milioni 9 waliopo nchini humo.
Balozi
Shidhani amesema kuwa nchi yake ina uelewa mkubwa zaidi kuhusu masuala ya
mafuta na gesi hivyo inaweza kuisaidia Tanzania kwa kuwajengea uwezo wataalamu
wake, halikadhalika Tanzania inaweza kuisaidia nchi yake katika masuala ya
madini kwa kuwa imepiga hatua zaidi katika eneo hilo.
“
Kuna maeneo mengi tunayoweza kushirikiana na Tanzania mfano hapa kuna umeme wa
ziada na sisi hivi karibuni tumefungua kituo cha kuzalisha hydrojeni na
Tanzania inaelekea huko hivyo kama kuna
fursa mpya tunaweza kushirikiana kwa karibu,” amesema Balozi Shidhani.
Ameongeza
kuwa nchi yake imeandaa jukwaa maalum kwa ajili ya kutoa fursa za ufadhili wa
masomo kwa Watanzania, pia ameahidi kuwa
nchi yake itachimba visima vya maji 20.
Na. Mwandishi wetu
0 Comments