Mabalozi wa nyumba 10 Kigoma watembelea miradi ya kimkakati

Karibu mabalozi mia sita wa Chama cha Mapinduzi CCM katika manispaa ya kigoma mjini wametembelea miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita katika mji wa kigoma ili kujionea maendeleo ya miradi hiyo.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kigoma Cde.Christopher Palangyo akizungumza na mabalozi hao amesema Chama kimeweka mkakati wa kuwawezesha mabalozi mkoa mzima kutembelea miradi ili kuona kazi ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan. 

"Watu wengi wakiwemo wana CCM wanahitaji kujionea ili tunaposema Mama aliahidi na ametekeleza watu waelewe kuwa ni kweli kazi imefanyika na inaonekana"alisema.

Mabalozi hao walipata nafasi ya kutembelea ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya kigoma ambayo tayari imeanza kutoa huduma huku majengo mengine yakiendelea kujengwa,Mradi mwingine uliotembelewa ni ujenzi na ukarabati wa uwanja wa ndege kigoma ambao unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 46.

Pia walitembelea mradi wa Ukarabati wa meli kongwe Duniani yenye zaidi ya miaka 100 MV. Liemba ambayo inakarabatiwa kwa zaidi ya Shilingi bilioni 36 pamoja na meli ya mafuta MT.Sangara ambayo inakarabatiwa kwa Shilingi bilioni nane pamoja na ujenzi wa soko la Mwanga unagharimu shilingi bilioni 16.

Mmoja wa mabalozi kutoka kata ya Kitongoni Hussein Abbas amesema hii ni mara ya kwanza mabalozi kupata nafasi ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Serikali na wamejionea kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali.

Akizungumzia ukarabati wa meli, mhandisi Ngenja Dave kutoka wakala wa meli nchini TASHICO amesema Ukarabati wa meli ya kusafirisha mafuta MT.Sangara umefikia asilimia 99 huku wa meli ya abiria na mizigo MV.Liemba ukarabati ukiwa umefikia asilimia 19. 

Naye msimamizi wa uujenzi na ukarabati wa uwanja wa ndege kigoma Mhandisi Mussa Njengwa amesema katika mradi huo kunajengwa jengo la abiria ghorofa moja, mnara wa kuongozea ndege, sehemu ya kuegesha magari na majengo mengine maalum kwa ajili ya uwanja huo.

Post a Comment

0 Comments